Rais Kikwete atoa mhadhara katika kituo cha Kimataifa cha Woodrow
Serikali
ya awamu ya nne inajivunia mafanikio iliyoyapata tangu kuingia
madarakani Mwaka 2005 na kuweka msingi imara wa nchi katika kutekeleza
Mkakati wa Maendeleo wa Mwaka 2025 (Tanzania Development Vision 2025)
ambao unalenga kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa kati
ifikapo Mwaka 2025.
Rais
Jakaya Mrisho Kikwete amesema hayo tarehe 3 Aprili, 2015 jijini
Washington DC wakati akitoa mhadhara katika kituo cha Kimataifa cha
Woodrow Wilson (Woodrow Wilson International Centre.
"Naamini mrithi wangu atayaendeleza na kujifunza kutokana na mafanikio haya na kuendeleza kutoka pale tutakapoachia" Rais
amesema na kuongeza kuwa pia anatarajia kuwa Tanzania itakuwa na sera
na sheria ya kusimamia Gesi na mapato yake kwa vile inatarajiwa kuanza
kupatikana ifikapo Mwaka 2020.
Katika
mhadhara huo uliohudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo Mabalozi, wasomi
na viongozi wa taasisi hiyo, Rais Kikwete ameelezea mafanikio na
changamoto katika uongozi wake wa miaka 10 katika elimu, siasa, uchumi
na maendeleo ya jamii.
"Najivunia
kuweza kuendelea kuliweka Taifa katika hali ya Umoja pamoja na
changamoto zote, tumepambana na vitisho pale vilipojitokeza na pia
tumetoa mchango mkubwa katika harakati za kisiasa zilizopelekea vyama
viwili kutiliana saini maridhiano na kupata muafaka Mwaka 2010".
Rais
ameelezea na kuongeza kuwa makubaliano hayo yalipelekea Zanzibar
kufanya uchaguzi kwa amani na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa baina
ya vyama vya CCM na CUF.
"Natumaini tutafanya uchaguzi huru, haki na amani ili niweze kumkabidhi Urais mrithi wangu katika hali ya utulivu" Rais ameongeza.
............Mwisho............
Imetolewa na;
Premi Kibanga
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Washington DC - Marekani
4 Aprili, 2015.