Kipindupindu Chalipuka kwa wakimbizi wa Burundi Walioko Katika Kambi ya Kigoma.
WAKATI
hali ya usalama nchini Burundi ikiwa bado tete, wakimbizi 558 walioko
katika kambi ya Nyarugusu mkoani Kigoma wanaugua ugonjwa wa
Kipindupindu.
Ugonjwa
huo ulilipuka hivi karibuni baada ya wakimbizi hao kuingia nchini
wakikimbia machafuko ya kisiasa yanayoendelea nchini humo.
Akizungumza
jana, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Steven Kebwe,
alisema hadi sasa wakimbizi 15 wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa
huo.
Alisema
tangu Aprili 24 mwaka huu wakimbizi 2,458 walikuwa wakiharisha na
kutapika na sampuli 11 kati ya 13 zilizochukuliwa juzi zilithibitisha
kuwa wanaugua ugonjwa wa kipindupindu.
“Tumeshirikiana
na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) na tayari tumepeleka timu ya
wataalamu ambao wametembelea maeneo ya Kagunga na Nyarugusu kutathmini
na kutoa elimu ya afya kwa umma.
“Tumefanya tathmini katika mikoa ya Kagera, Geita na Katavi ambayo inapakana na Burundi,” alisema Dk. Kebwe.
Alisema
wamepeleka dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya dharura pamoja na
kuanzisha mfumo wa kufuatilia magonjwa yakiwemo ya mlipuko katika maeneo
yaliyoathiriwa.
Kwa
mujibu wa Dk. Kebwe, ugonjwa wa kipindupindu unatokana na kula chakula
au kunywa kinywaji chenye vimelea vinavyosababisha kuharisha ambavyo
hupatikana kwenye kinyesi, matapishi au majimaji kutoka kwa mgonjwa.
Alizitaja
dalili za ugonjwa huo kuwa ni kuharisha mfululizo bila maumivu ya
tumbo, kinyesi cha majimaji kinachofanana na maji ya mchele, kutapika
mfululizo, kuishiwa nguvu na kwamba ndani ya masaa sita kama hakuna
huduma mgonjwa anaweza kupoteza maisha.
Kuhusu
gharama za matibabu, alisema wametoa kwenye akiba ya magonjwa ya
dharura na mlipuko lakini zitarejeshwa baadaye na Shirika la Umoja wa
Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR).
Alitoa
wito kwa wananchi kuzingatia usafi wa mazingira, usafi wa vyoo, kunywa
maji safi na salama, kunawa mikono kwa sabuni kabla na baada ya kutoka
chooni na kusafisha vyakula.