Waziri Sitta Awatimua Vigogo wa Kampuni ya Reli nchini (TRL)..... Madeni Kipande Wa TPA Kafukuzwa Kazi Rasmi
SERIKALI
imewasimamisha kazi karibu viongozi wote wakuu wa Kampuni ya Reli
nchini (TRL), kwa kile kilichoelezwa kuwa hujuma ya mabilioni ya
shilingi yaliyotumika kununua mabehewa chakavu.
Waliosimamishwa
ni pamoja na Mkurugenzi Mtendaji, Kipallo Kisamfu, Mhandisi Mkuu wa
Mitambo, Ngosomwile Ngosomiles, Mhasibu Mkuu, Mbaraka Mchopa, Mkaguzi
Mkuu wa Ndani, Jasper Kisiraga na Meneja Mkuu wa Manunuzi wa kampuni
hiyo, Ferdinand Soka.
Wakati
hayo yakiwakuta hao, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari (TPA),
Madeni Kipande aliyekuwa amesimamishwa kazi kutokana na tuhuma
mbalimbali, sasa amefukuzwa rasmi.
Hayo
yaliwekwa hadharani jana na Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta
alipokutana na waandishi wa habari na kutoa taarifa ya uchunguzi kuhusu
ununuzi wa mabehewa machavu katika Kampuni ya Reli nchini.
Sitta,
mmoja wa wanasiasa wakongwe aliyeshika nyadhifa mbalimbali serikalini
ikiwa ni pamoja na uwaziri tangu enzi za utawala wa Awamu ya Kwanza
chini ya Mwalimu Julius K. Nyerere, alisema mbali ya madudu
yaliyoonekana katika kamati iliyoundwa na mtangulizi wake katika wizara
hiyo, Dk Harrison Mwakyembe, waligundua mambo mengi Jumatatu wiki hii.
Yaliyogunduliwa
ni pamoja na ukiukwaji mkubwa wa masharti ya mkataba wa ununuzi wa
mabehewa hayo, kwani mzabuni alilipwa fedha zote, tofauti na taarifa za
awali iliyoonesha malipo yangefanyika kwa awamu.
“Hivyo
wizara ina maoni kwamba mazingira ya utekelezaji wa mkataba huu yana
dalili za hujuma kwa TRL na kwa nchi yetu na siyo uzembe,” alisema Sitta.
Akifafanua
hilo alisema TRL iliagiza mabehewa ya mizigo 274 ambapo zabuni
ilikwenda kwa Kampuni ya Hindustan & Industrial Engineering Limited
ya India, ambapo katika uagizwaji wa mabehewa hayo kulikuwa na uzembe
katika ufuatiliaji kiwandani, pamoja na uzembe katika kuyapokea yakiwa
mabovu.
Alisema
mabehewa hayo yalipofikia 150 aliyazuiwa, hivyo 124 yakawa bado
hayajafika nchini. Sitta alisema kwa mujibu wa taarifa alizonazo ilibidi
mpaka sasa asilimia 50 ya gharama ya mabehewa hayo iwe imeshalipwa,
lakini kinyume chake nyaraka zinaonyesha mpaka sasa pamoja na kuzuiwa
kwa mabehewa 124 mzabuni huyo ameshalipwa asilimia 100.
“Huu ni uzembe, ni hujuma kama kiongozi sitamstahi yeyote atakayekuwa sehemu ya hujuma,” alisema Sitta.
Alisema
kutokana na hali hiyo ameagiza kwamba uchunguzi wa kubaini uwezekano wa
hujuma ufanyike, hivyo amemwelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi,
Dk Shaaban Mwinjaka asimamie kuundwa kwa kamati ya uchunguzi.
Alisema
kamati hiyo itaongozwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa
(TAKUKURU), Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi katika Sekta ya Umma (PPRA),
na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Sitta
ametoa wiki tatu kuanzia Jumatatu ijayo Aprili 20, mwaka huu kuchunguza
na kukamilisha kazi. Katika kipindi hicho, viongozi wakuu wa kampuni
hiyo ya reli wanaowajibika na mkondo wa kashfa hiyo ya uagizaji na
malipo ya ununuzi wa mabehewa hayo wote wamesimamishwa kupisha uchunguzi
huo.
Aidha,
alisema tangu mwanzoni mwa mwaka huu serikali ilikuwa ikifanyia kazi
tuhuma zinazohusu mabehewa mabovu ya mizigo yaliyoagizwa kutoka India na
TRL, baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa tuhuma hizo na kamati
iliyoundwa na Mwakyembe, aliagiza bodi ya wakurugenzi ya TRL ipitie
taarifa hiyo na maelezo ya suala zima la mabehewa hayo.
Alisema
katika uchunguzi huo ilibainika kuwa mabehewa mengi kati ya
yaliyoagizwa yana kasoro, pia kulikuwa na uzembe katika uagizaji na
ufuatiliaji kiwandani yalipokuwa yanatengenezwa na kulikuwa na uzembe
katika kuendelea kuyapokea mabehewa hayo pamoja na ubovu wake
kujulikana.
Alisema
amemteua Elias Mshana kukaimu nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji hadi hapo
uchunguzi utakapokamilika. Pia ameagiza bodi ya wakurugenzi ya TRL
ikutane kuteua watumishi wenye sifa kukaimu nafasi wanaozishikilia
waliosimamishwa kazi.
Kipande wa TPA
Akizungumza
suala la Kipande, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari aliyekuwa
amesimamishwa kazi tangu Februari 16, mwaka huu ili kupisha uchunguzi wa
tuhuma mbalimbali dhidi yake, Sitta alisema Tume aliyoichagua
ilikamilisha kazi yake Machi 20, na kumkabidhi taarifa ya uchunguzi wao
Machi 24 kwa hatua zaidi.
“Baada
ya kuisoma taarifa ya tume na hatimaye kushauriana na taasisi
mbalimbali zinazohusika na masuala haya, tumeridhika pasipo mashaka
yoyote kwamba isingefaa Madeni Kipande kuendelea na kazi ya kuongoza
Mamlaka ya Bandari.
“Hii
ni kutokana na kuridhika na utawala mbovu aliouendesha uliosababisha
manung’uniko mengi miongoni mwa wateja na wadau wa bandari na mgawanyiko
mkubwa wa wafanyakazi,” alisema Sitta.
Alisema kutokana na hali hiyo, serikali imeamua kumrejesha Kipande Idara Kuu ya Utumishi ili aweze kupangiwa majukumu mengine.
“Kipande
ameonekana hafai kuongoza bandari ana maamuzi ya pupa, yasiyofuata
taratibu pia yenye karaha. Tulichunguza uwezo wake wa kuendesha mamlaka
ya bandari sasa kishapwaya inabidi arudishwe utumishi.
Hapa hatujachunguza masuala ya jinai, bali uwezo wa kutenda kazi,” alisema Sitta.
Tangu
kusimamishwa kwa Kipande ambaye alikuwa anakaimu nafasi ya Mkurugenzi
Mkuu, Ephraim Mgawe aliyekuwa ameondolewa kutokana na tuhuma mbalimbali,
nafasi hiyo sasa inashikiliwa na Awadhi Massawe aliyepata baraka za
Waziri Sitta na kuendelea kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu TPA.
POSTED BY; RASHID HAMZA