Wanaharakati, Bloggers, Wamtaka JK kutotia saini Miswada ya dharura iliyojadiliwa Bungeni
Mkurugenzi
mtendaji wa Kampuni ya Jamii Media, Maxence Melo, (wamiliki wa mitandao
maarufu ya mijadala kwa jamii kupitia mitandao ya jamii, JamiiForums na
FikraPevu hapa nchini) akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam (hawako pichani) wakati wa kutoa tamko la pamoja lililotolewa na
Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu
KUFUATIA
kitendo cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha miswada
miwili ukiwemo Muswada wa Sheria ya Takwimu ya Mwaka 2015 na pamoja na
Sheria ya Makosa ya Mtandaoni bila kurekebisha au kuviondoa vifungu
vinavyokwenda kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Muungano ya
mwaka 1977, wanaharakati wa kutetea haki za binadamu kwa pamoja
wamelaani vikali kupitishwa kwa miswada hiyo bungeni mjini Dodoma.
Tamko la
baadhi ya Wanachama wake wakiwemo Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
(LHRC), Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), SIKIKA, Mtandao
wa Jinsia-TGNP, Kampuni ya Jamii Media ambao ni wamiliki wa mitandao
maarufu nchini inayoendesha mijadala kwa jamii (JamiiForums na
FikraPevu) pamoja na Mtandao wa Watoa Huduma za Msaada wa Kisheria
(TANLAP) wameeleza kushtushwa kwa hatua hiyo na kwamba muswada wa
takiwmu umetoa madaraka makubwa kwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu kama
Kitovu cha utoaji wa Takwimu nchini.(P.T)
Taarifa
iliyotolewa leo Aprili 2, 2015 na Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao huo,
Onesmo Olengurumwa (FikraPevu imepata nakala), imesema muswada wa Sheria
ya Makosa ya Mtandaoni unaainisha makosa yanayohusiana na matumizi ya
mfumo wa kompyuta na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na kwamba
inawabana sana watumiaji na hivyo kama Rais atasaini muswada huo
wananchi wengi wataumia kuliko inavyofikiriwa na watu wengi.
"Sheria
hii ya Mitandao itaminya kwa kiasi kikubwa uhuru wa wananchi kuwasilina
na kupashana habari kama itasainiwa bila marekebisho. Ni dhahiri sheria
hii imelenga kufuta kabisa matumizi ya mitandao ya kijamii kama vile
Facebook, WhatsApp,JamiiForums, twitter, blogu n.k. Kupitishwa kwa
sheria hii bila kufanyiwa marekebisho kutasabisha watanzania wengi
kuwekwa hatiani bila sababu, lakini pia kutaondoa kabisa uhuru wa habari
nchini"ilieleza sehemu ya tamko hilo.
Mbali na
hayo taarifa hiyo imebainisha kuwa wanaharakati hao wameona kuwa sheria
hiyo imetungwa kwa uharaka kwa malengo yaliyofichika hasa kipindi hichi
cha vuguvugu la uchaguzi bila kuzingatia madhara yake kwa jamii ambayo
hivi sasa inatumia kwa wingi mitandao ya kijamii kuwasiliana na kujadili
mambo muhimu na kwamba mamlaka waliyopewa wakuu wa Vituo vya Polisi na
Waziri mwenye dhamana yatawaumiza watanzania walio wengi hivyo ni vyema
suala hilo likaangaliwa kwa jicho la pili ili mhimili wa Mahakama uweze
kupata heshima yake.
Hata
hivyo, wanaharakati hao wamewataka Watanzania wote na watumiaji wa
mitandao ya kijamii kumtaka Rais Jakaya Kikwete, kusitisha kupitisha
muswada huo, bali atoe muda kwa Watanzania kutoa maoni na mapungufu ya
sheria hizi kwa ajili ya marekebisho mbalimbali.
Wakizungumzia
kuhusu Muswada wa Takwimu uliopitishwa na Bunge wamesema muswada huo
unataka taasisi zote za Serikali, Mashirika Binafsi, Taasisi za Elimu ya
Juu, Vyuo vikuu na Taasisi za Utafiti kutokuwa na uhuru wa kutoa
matokeo ya tafiti wanazozifanya bila ya kibali au ridhaa ya Ofisi ya
Takwimu hali ambayo itakuwa inawanyima haki wananchi kujua mambo
yanayoendelea kwenye taifa lao.
"Rais
Jakaya Kikwete, amekuwa akijahidi kuanzisha progamu mbalimbali za uwazi
na ukweli kama vile Open Government Partnership na mengineyo. Hivyo
tunamsihi sana asikubali kutia sahihi sheria hii ya Takwimu kwa kuwa
inakwenda kinyume na Misingi ya Utawala Bora pamoja na vifungu vya
kikatiba. Asitishe kutia saini kwenye sheria hii hadi itakapofanyiwa
marekebisho ya vifungu vinavyolalamikiwa"
Wakati
Taifa likihubiri kuzingatia uhuru wa vyombo vya habari na haki ya kupata
habari, wamesema wanashangazwa kuona serikali inazidi kuongeza sheria
kandamizi dhidi ya uhuru wa habari kutokana na sheria kulenga kuua uhuru
wa habari kwa kuweka adhabu ya faini isiyopungua milioni 10 na kuifungo
cha miaka miwili kwa kuchapisha taarifa au takwimu za uongo au za
upotoshaji.
Wamewataka
wadau wote wa masuala ya utafiti nchini, vyombo vya habari, wananchi
wote, wadau wa maendeleo na Wabunge, kutumia vyombo vyao vizuri kwa muda
huu ili kuonyesha ubaya wa sheria katika kazi za utafiti chini na hata
katika uhuru wa habari nchini.
Mtandao wa Mabloggers walalamika
Mtandao
wa Waandishi wa habari kupitia mitandao nchini, Tanzania Bloggers
Network (TBN) wamemtaka Rais Kikwete, kutopitisha muswada wa Sheria ya
Makosa ya Mtandao, 2015 unaokandamiza uhuru wa mawasiliano mitandaoni na
kwamba umoja huo ulishtushwa na kitendo cha bunge kukubali kuupitisha,
kitendo ambacho hakikutarajiwa kutokana na kuwa mitandao bado ni kitu
kipya nchini hivyo walihitaji maridhiano na wadau na elimu kati ya raia
na Serikali ili wengi watambue yapi ni makosa kwa kutumia mitandao na
yapi yanakubalika.
"Kimsingi
TBN haipingi Tanzania kuwa na Sheria ya Makosa ya Mtandao bali inaiomba
Serikali kuwashirikisha wananchi na hasa wadau wa habari na
wanamitandao ya jamii ili kuridhiana kwa vipengele ambavyo vinaonekana
kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari. Na hatimaye kutokana na sheria
isiyo na viashiria kandamizi juu ya uhuru wa kupata na pokea
taarifa...tumeshuhudia watetezi wa haki za binadamu pamoja na
wawakilishi wa watumiaji wa Mtandao wa intaneti nchini wakitoa sababu
zenye uzito" ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa
hiyo imesema pia kuwa wao kama waandishi wengine ulimwenguni wanafuata
maadili ya kazi zao ikiwa ni pamoja na kutunza usiri wa chanzo cha
habari pale inapotakiwa lakini wanashangazwa na katika sheria hiyo wao
kama bloggers, sheria hiyo inakiuka kipendele hicho kwa kuwalazimisha
kutaja vyanzo vya habari.
"Tunakukumbusha
kuwa mwananchi wa kawaida anayetumia mtandao wa intaneti kuwa hayuko
salama kwani sheria hii inamlazimisha mtoa huduma wa mtandao kutoa
taarifa za wateja wake jambo ambalo linahatarisha uhuru wa kutoa na
kupokea habari"
Tangu kutolewa taarifa ya kuwepo kwa miswada hiyo katika Bunge la 10 na mkutano wa 19 wananchi mbalimbali katika mitandao ya kijamii ukiwemo mtandao wa JamiiForums wamesema sheria hiyo inaonekana imeletwa kwa malengo ya kupunguza matumizi mabaya ya mitandao kutokana na kutokuwepo na busara ya serikali kushishirika umma wa Watanzania kabla ya kuupitisha.
Chanzo:http://www.fikrapevu.com/
POSTED BY;ANNASTAZIA RH & HASSAIN MTUNDA
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni