Mwanafunzi auawa baada ya kukutwa na barua ya mapenzi
MWANAFUNZI wa Kidato cha Pili, Jofrey Robert Mwakatenya (15)
anatuhumiwa kuuawa kikatili na baba yake mzazi, Robert Mwakatenya (35)
baada ya kumkuta akiwa na barua ya mapenzi, inayodaiwa aliandikiwa na
rafiki wake wa kike.
Mzazi huyo ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa eneo la Majengo ‘D’
Manispaa ya Sumbawanga, anadaiwa kumwadhibu mwanafunzi huyo, ambaye ni
mtoto wake wa kwanza kwa kupiga ngumi na mateke mfululizo kwa zaidi ya
saa tatu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa , Jacob Mwaruanda alithibitisha tukio
hilo, lilitokea usiku wa kuamkia Jumapili iliyopita. Alisema bado
wanamtafuta mtuhumiwa huyo kwani baada ya kufanya kitendo hicho
alitokomea.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mwenyekiti wa Serikali
Majengo D, Antony Nyambo alidai kuwa mzazi huyo alikuwa na tabia ya
kumwadhibu mwanawe huyo, akimtuhumu kuwa ni mtoro wa shule .
“Nilitaarifiwa juu ya kisa hiki Jumapili saa mbili asubuhi baada ya
kutoka katika ibada na raia mwema, ndipo niliamua kufika nyumbani kwa
marehemu, nilimkuta akiwa amelazwa chumbani, nilipomfunua niliona akiwa
ametapakaa vumbi mwili mzima huku akiwa amevaa nguo ya ndani tu,” alidai
mwenyekiti huyo wa mtaa.
Inadaiwa kuwa usiku huo wa tukio, mtuhumiwa alianza kumwadhibu
kumpiga ngumi na mateke kuanzia saa mbili usiku hadi usiku wa manane.
Mtoto huyo baada ya kupata kipigo hicho, alizimia ambapo baba yake
alimwagia maji mwilini hadi akazinduka, kisha akamwamuru alale chumbani
humo pamoja na mdogo wake.
Mzazi wa mtoto huyo alidamka alfajiri na kwenda kwenye chumba walicholala watoto hao na kugundua kuwa Jofrey alikuwa mfu.
“Ndipo baba huyo alipoaga nyumbani hapo, akidai kuwa anaenda kutafuta
gari ili Jofrey aweze kupelekwa hospitalini kwa matibabu. Mzazi huyo
hakurudi tena nyumbani kwake hadi sasa,” alibainisha.
CHANZO Mpekuzi blog
POSTED BY ANNASTAZIA JR
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni