Jumapili, 3 Mei 2015

UGAIDI Watikisa Tena Morogoro......Watu Watano Wajeruhiwa Kwa Bomu, Vijana Wawili Wanaswa Na Kutoroka Kimafia

WATU watano akiwemo dereva wa gari linalotumiwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kilombero, David Ligazio ,Novatus Ngope (47), wamejeruhiwa vibaya na shambulio la kitu kinachodhaniwa ni bomu la kutupwa na mkono kutoka kwa watu wawili wasiofahamika walipokuwa kwenye sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani juzi.
 
Bomu hilo liliwajeruhi watu hao walipokuwa kwenye maadhimisho hayo yaliyofanyika katika kijiji cha Msolwa Ujamaa ,Kata ya Sanje ,wilayani Kilombero, mkoani Morogoro.
 
Dereva huyo anayeishi Ifakara anayeendesha gari la halmashauri lenye namba za usajili SM 10632 na wenzake baada ya kulipuliwa na bomu walikimbizwa Kituo cha Afya cha Nyandeo kilichopo Tarafa ya Kidatu ,baadaye walihamishiwa Hospitali Mtakatifu Kizito iliyopo Mikumi,wilayani Kilosa.
 
Mkuu wa wilaya ya Kilombero, Lephy Gembe alithibitisha jana kwa njia ya simu alipozungumza na mwandishi na kusema tukio hilo lilitokea majira ya saa 2:00 usiku wa Mei Mosi mwaka huu eneo la Kijiji cha Sanje.
 
Alisema vijana wawili wanaotuhumiwa kurusha mlipuko huo baada ya kuwajeruhi watu hao watano, walifanikiwa kukimbia kutoka eneo la tukio na Polisi inaendelea kuwasaka ili watiwe nguvuni.
 
Hata hivyo alisema, bado mpaka sasa taarifa kamili kuhusu chanzo na mazingira yake hakijafahamika na kwamba timu ya askari iliwasili eneo la tukio kwa ajili ya kukusanya taarifa na kuwasaka wahalifu hao.
 
Alisema inawezekana huo ni muendelezo wa matukio ya kihalifu kufuatia kukamatwa kwa watuhumiwa 12 waliokutwa na milipuko hatari na vitu mbalimbali zikiwemo sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ)Aprili 14, mwaka huu katika Kata hiyo ya Kidatu, wilayani Kilombero.
 
"Ni wiki chache zilizopita tumewakamata watu 12 na milipuko hatari na sare za jeshi , inawezekana kundi hili la kihalifu ni kubwa na wengine wameendelea kujificha msituni,” alisema Mkuu wa wilaya.
 
Tukio la mlipuko huo umetokea karibu na eneo ambapo hivi karibuni ,Polisi iliwakamata watu kumi wakiwa na milipuko 30,sare za jeshi ,majambia, risasi ,bendera zenye maandishi ya lugha ya kiarabu ,vitabu na madaftari wakiwa ndani ya msikiti wa Suni, Kidatu wilayani humo.
 
Kwa mujibu wa Mkuu wa wilaya hiyo, katika tukio hilo watu hao waliojeruhiwa ni pamoja dereva wa gari la halmashauri ya wilaya ambalo linatumiwa na Mwenyekiti wake.
 
“Pamoja na kumjeruhi dereva huyo pia gari limevunjwa kabisa kioo cha nyuma na kupasuliwa cha mbele kutokana na mlipuko huo,” alisisitiza Mkuu wa wilaya.
 
Hata hivyo alisema, timu ya maofisa wa vyombo vya ulinzi na usalama vya wilaya hiyo tayari vimelekea eneo la tukio hilo kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kina.
 
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Ligazio , akielezea tukio hilo alisema kuwa siku hiyo alikuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya siku ya wafanyakazi ngazi ya kata ya Sanje, akiwa ni diwani wa kata hiyo.
 
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo wa halmashauri, muda mfupi baadaye alikuja Mwenyekiti wa kitongoji hicho Joseph Mhenga akiambatana na vijana wawili .
 
Hata hivyo alisema, mwenyekiti huyo wa kitongoji kabla ya kufikishwa kwake alishawahoji walipotokea na walionekana si wenyeji wa eneo hilo kufuatia hofu walizokuwa wakizionesha.
 
Hata hivyo alisema vijana hao waliletwa kwake na mwenyekiti huyo wa kitongoji ili kutaka ushauri kuhusu vijana hao na alimwambia vijana hao wafikishwe katika kituo cha Polisi Kidatu kwa utaratibu mwingine wa kipolisi.
 
Kabla ya kupelekwa kituoni , vijana hao walifanyiwa upekuzi na askari wa mgambo, Thomas Manjole(54) ,mkazi wa Msolwa na walibainika kuwa na bomu.
 
Hata hivyo alisema , vijana hao walilitoa bomu hilo kiunoni na kulirusha kwenye gari la halmashauri ambalo linatumiwa na Mwenyekiti wa halmashauri hiyo.
 
Bomu hilo lilipolipuka likamjeruhi dereva wake aliyekuwa ndani ya gari pamoja na wengine wanne akiwemo askari mgambo.
 
 Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa halmashauri hiyo ambaye hakuwemo ndani ya gari aliwataja majeruhi hao ni dereva wake ,askari mgambo alikuwa akiwapekuwa vijana hao, Amos Msopole(29) na Azama Naniyunya(59) wote wakazi wa Kijiji cha Msolwa Ujumaa.
 
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji wa Kata ya Sanje , Hawa Ndachuwa ,alidai siku ya tukio watu wawili walikodi bodaboda kutoka Kata ya Kidatu na kuomba wapelekwe eneo la Kata ya Mkula .
 
Hata hivyo alidai kuwa, walipofika Msolwa Ujamaa, dereva wa bodaboda aliwashuku watu hao na kutaka aongezewe fedha za malipo kwani mapatano hayakulingana na umbali.
 
Alisema watu hao walikubali kumuongezea fedha na walimwomba kuwaonesha sehemu ya kutolea fedha na kuwapeleka eneo la kutolea fedha na kwamba mwendesha bodaboda huyo aliamua kuuarifu uongozi wa serikali ya kitongoji hicho.
 
Kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji wa Kata hiyo, baada ya wananchi kuwaona watu hao walipatwa na mshtuko kutokana na mavazi waliyovaa na kisha kuwaweka chini ya ulinzi na kuanza kuwapekua na ulifanyika chini ya ulinzi wa askari mgambo wa kijiji.
 
Hivyo alisema, wakati wanaendelea kupekuliwa, mtuhumiwa mmoja alikutwa na viberiti vya gesi na wakati upekuzi ukiendelea mtuhumiwa mwingine aligoma kutoa ushirikiano hali iliyowatia hofu zaidi wananchi ambapo walimwona akiwa na kitu amekihifadhi kiunoni.
 
Ofisa Mtendaji huyo alisema, wakati wanaendelea kupekuliwa mtuhumiwa wa kwanza alifanikiwa kukimbia na wakati wanajiandaa kumdhibiti wa pili alitoa kitu kama bomu na kurusha lilipo hilo gari la mwenyekiti na kutoa mlipuko mkubwa na yeye pia kutoroka.
 
Kutokana na mlipuko huo , askari mgambo Manjole ndiye alijeruhiwa vibaya kwa kuvunjika mguu na mkono huku dereva wa mwenyekiti Novatus akiumia begani na wote wanne kuchukuliwa na kupelekwa katika kituo cha afya cha Nyandeo .
 
Hata hivyo alisema , Polisi walifika eneo la tukio na kuwasiliana na wataalamu wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) waliopo eneo ya Kidatu ili kubaini bomu hilo huku wakiendelea kuwasaka watuhumiwa.
 
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mtakatifu Kizito, Maximilian Mwenda, alithibisha kupokea majeruhi wanne wa tukio hilo, kati yao mmoja akiwa na hali mbaya ambapo wengine wanaendelea kupatiwa matibabu na hali zao zinaendelea vyema.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni