Jumatano, 20 Mei 2015

Kipindupindu Chalipuka kwa wakimbizi wa Burundi Walioko Katika Kambi ya Kigoma.


WAKATI hali ya usalama nchini Burundi ikiwa bado tete, wakimbizi 558 walioko katika kambi ya Nyarugusu mkoani Kigoma wanaugua ugonjwa wa Kipindupindu.
 
Ugonjwa huo ulilipuka hivi karibuni baada ya wakimbizi hao kuingia nchini wakikimbia machafuko ya kisiasa yanayoendelea nchini humo.
 
Akizungumza jana, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Steven Kebwe, alisema hadi sasa wakimbizi 15 wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.
 
Alisema tangu Aprili 24 mwaka huu wakimbizi 2,458 walikuwa wakiharisha na kutapika na sampuli 11 kati ya 13 zilizochukuliwa juzi zilithibitisha kuwa wanaugua ugonjwa wa kipindupindu.
 
“Tumeshirikiana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) na tayari tumepeleka timu ya wataalamu ambao wametembelea maeneo ya Kagunga na Nyarugusu kutathmini na kutoa elimu ya afya kwa umma.
 
“Tumefanya tathmini katika mikoa ya Kagera, Geita na Katavi ambayo inapakana na Burundi,” alisema Dk. Kebwe.
 
Alisema wamepeleka dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya dharura pamoja na kuanzisha mfumo wa kufuatilia magonjwa yakiwemo ya mlipuko katika maeneo yaliyoathiriwa.
 
Kwa mujibu wa Dk. Kebwe, ugonjwa wa kipindupindu unatokana na kula chakula au kunywa kinywaji chenye vimelea vinavyosababisha kuharisha ambavyo hupatikana kwenye kinyesi, matapishi au majimaji kutoka kwa mgonjwa.
 
Alizitaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni kuharisha mfululizo bila maumivu ya tumbo, kinyesi cha majimaji kinachofanana na maji ya mchele, kutapika mfululizo, kuishiwa nguvu na kwamba ndani ya masaa sita kama hakuna huduma mgonjwa anaweza kupoteza maisha.
 
Kuhusu gharama za matibabu, alisema wametoa kwenye akiba ya magonjwa ya dharura na mlipuko lakini zitarejeshwa baadaye na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR).
 
Alitoa wito kwa wananchi kuzingatia usafi wa mazingira, usafi wa vyoo, kunywa maji safi na salama, kunawa mikono kwa sabuni kabla na baada ya kutoka chooni na kusafisha vyakula.

Mabadiliko mengine kuhusu uchaguzi mkuu Burundi!!

NKUU
Hali bado si shwari Burundi..hii inatokana na machafuko ya kisiasa yanayoendelea baada ya Rais aliyeko madarakani Pierre Nkurunziza kutaka kuwania kwa muhula wa tatu mfululizo.
Baada ya kutofikia makubaliano ikiwemo jaribio la kutaka kumpindua lililofanywa wiki moja iliyopita kushindikana huku watu wakiendelea kaandamana kushinikiza aondoke.
Rais huyo amehairisha uchaguzi wa ubunge kwa siku kumi .
Msemaji wake Willy Nyamitwe amesema Rais huyo ameahirisha uchaguzi wa Ubunge kwa muda wa siku 10 kufuatia jaribio la mapinduzi.
Awali uchaguzi huo ulipangwa kufanyika Mei 26 na sasa utafanyika June 2 na umeahirishwa ili kupata muda wa kuwasikiliza washirika wa kimataifa pamoja na tume ya uchaguzi.
Hadi  sasa tarehe rasmi ya uchaguzi wa Urais uliopangwa kufanywa Juni 26 haijabadilika.

Jumapili, 3 Mei 2015

Taarifa Muhimu Kutoka CHADEMA


Taarifa inatolewa kwa vyombo vya habari kuwa kuwa Kamati Kuu ya Chama, chini ya Mwenyekiti wake Freeman Mbowe, itakutana Mei 3-4, katika kikao chake cha kawaida kwa mujibu wa Katiba ya Chama.
 
Katika kikao hicho cha siku mbili kitakachofanyika jijini Dar es Salaam, pamoja na masuala mengine ya kitaifa kuhusu hali ya kisiasa nchini kwa ujumla na mengine mahsusi yanayohusu uendeshaji wa chama, KK itapokea taarifa, kujadili na kufanya maamuzi kuhusu;
 
1. Maandalizi ya Chama kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
 
2. Taarifa ya ziara ya mafunzo kwa timu za kampeni, viongozi wa serikali za mitaa na chama, kukiandaa chama kushinda
dola na kuongoza serikali baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
 
3. Taarifa za utendaji wa chama kupitia kanda zote 10, Tanganyika na Zanzibar.
 
4. Taarifa ya maendeleo ya mikakati ya kushiriki uchaguzi mkuu kwa kushirikiana na vyama 4 vinavyounda UKAWA.
 
5. Taarifa za mwenendo wa shughuli ya uandikishaji wa wapiga kura (upya) katika daftari la kudumu kwa teknolojia ya Biometric Voters Registration (BVR) na hatma ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.
 
Imetolewa  Jumamosi, Mei 2, 2015 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara a Habari na Mawasiliano-CHADEMA

Vurugu Burundi: Wakimbizi 800 Waingia Nchini



WAKIMBIZI 800 kutoka nchini Burundi wameingia nchini kupitia mkoani Kigoma huku wengine 87 wakirejeshwa nchini mwao baada ya kuingia nchini kwa kupitia wilayani Ngara mkoani Kagera.
 
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi, Isack Nantanga alisema wakimbizi hao wameingia nchini kwa makundi madogo madogo na watahifadhiwa kwa muda katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu.
 
Akizungumza na mtandao  huu jana,Nantanga alisema wakimbizi wanaofikia 800 wameshaingia nchini huku walioingia kupitia mkoani Kagera ilibidi warejeshwe walipotoka kutokana na kukiuka sheria za kimataifa kwa wakimbizi kuingia nchi nyingine wakivuka nchi moja.
 
Walianzia Rwanda.
Alisema hawapokei wakimbizi wanaotokea Rwanda kutokana na kuwa sheria za kimataifa haziruhusu wakimbizi kuvuka nchi moja ndiyo maana waliwarejesha wakimbizi hao. 
 
Alisema kati ya wakimbizi hao waliopokelewa mkoani Kigoma wameingia kupitia vijijini ambapo serikali za vijiji wanawapokea na kuwahoji kisha kuwapeleka kigoma mjini kwenye kituo maalum.
 
Alisema serikali za vijiji na wilaya kwa kushirikiana na halmshauri wamekuwa wakaifanya kazi ya kuwahoji kujua sababu hasa ya kuwafanya wakimbilie nchini humu kwani isije kutumika vurugu za Burundi watu kuingia nchini.
 
“Serikali kwa kushirikiana na Shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) baada ya kuwahoji na kuwapa misaada muhimu wanaobainika kupata hifadhi wana mpango wa kuwapeleka kwenye kambi ya Nyarugusu kwa muda,”alisema.
 
Msemaji huyo alisema baada ya kuhifadhiwa katika kambi hiyo mipango inaendelea kufahamu njia nyingine za kuwahifadhi.
 
 Kutoka Kigoma 
Mratibu wa idara ya wakimbizi ya Wizara ya Mambo ya ndani kanda ya Magharibi Kigoma,Tonny Laiser amesema kuwa wakimbizi hao wameanza kuingia mkoani Kigoma wakipitia maeneo tofauti ya mpaka kati ya mkoa huo na nchi ya Burundi.
 
Wengi wa wakimbizi hao wametokea mji wa Bujumbura na wameingia Kigoma kwa usafiri wa boti kupitia bandari ndogo ya Kibirizi mjini Kigoma.
 
Inaelezwa kuwa kundi kubwa la wakimbizi liliingia nchini juzi katika mpaka wa Tanzania na Burundi kwenye kijiji cha Kagunga mwambao wa kaskazini wa ziwa Tanganyika ambapo kundi la wakimbizi 200 waliingia kupitia kijiji hicho.
 
Tayari wakimbizi 68 ambao waliingia na kufikia kambi ya muda ya NMC kibirizi mjini Kigoma wamepelekwa kwenye kambi ya Nyarugusu wilayani Kasulu ambayo kwa sasa ndiyo kambi pekee mkoani Kigoma inayohifadhi wakimbizi.
 
Akizungumzia kuingia kwa wakimbizi mkoani humo Mkuu wa mkoa Kigoma, Issa Machibya alisema kuwa wameanza kupokea wakimbizi kutoka vijiji mbalimbali vya wilaya za Buhigwe,Kasulu na Kibondo ambao wanakimbia hali ya machafuko nchini Burundi.
 
Machibya alitaja maeneo ambayo hadi sasa yamekuwa yakipokea wakimbizi hao kuwa ni pamoja na Kijiji cha Kagunga wilaya ya Kigoma, Muyama,Kibande na Kilelema ambavyo vyote vipo katika wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma.
 
Kuingia kwa wakimbizi wa Burundi nchini Tanzania kunatokana kuanza kwa machafuko nchini humo kati ya wananchi wanaopinga kitendo cha Rais wa nchi hiyo, Pierre Nkurunzinza kuongoza muhula wa tatu wa uongozi dhidi ya polisi na wanajeshi wanaomtii raisi huyo.
 
Kwa siku mbili mfululizo kumekuwepo na taarifa za kuchomwa mwa mabasi mawili ya abiria na moja kulipuliwa kwa bomu la kurushwa kwa mkono huku kukiwa na vifo vya watu kadhaa kutokana na makabiliano ya waandamanaji na polisi.
 
Wageni wamekuwa wakizuiliwa kuingia mji mkuu wa Burundi, Bujumbura ambako kwa kiasi kikubwa maandamano ya kupinga hatua ya Rais Nkurunzinza kuongoza muhula wa tatu yanaendelea ambapo kwa sasa maandamano hayo yameanza kusambaa mikoa ya jirani na mji Mkuu wa Bujumbura.
 
Kwa upande wa wilaya ya Ngara, Mkuu wa wilaya ya Ngara, Costantine Kanyasu amesema Serikali ya Tanzania imewarejesha wakimbizi 87 waliotokea Burundi kwa madai kuwa wamekimbia mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.
 
Wamerejeshwa kutokana na kutofuata taratibu za kuomba hifadhi ya ukimbizi. Aliuambia  mtandao huu jana mjini Ngara kuwa kuanzia Aprili 29 mwaka huu mpaka Mei mosi waliingia wakimbizi 87 kutoka Burundi kupitia njia za panya bila kufuata utaratibu ambapo walipokamatwa na kuhojiwa walidai wanakimbia mapigano yanayoendelea nchini mwao.
 
“Tulipopata taarifa tuliwasaka na kuwakamata kisha tukawasiliana na Serikali yao ambapo walituhakikishia usalama wa watu wao na kutuomba tuwarejeshe nchini mwao kwa sababu hali ni shwari na sisi jana tuliwarejesha kwao ambapo walipokelewa na uongozi wa Serikali yao,”alisema Kanyasu.
 
Alisema baada ya kuwarejesha makwao hakuna taarifa nyingine za kuonekana wakimbizi wakiingia wilayani huo kwani wananchi kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama wanahakikisha kila anayejipenyeza wanamtambua na kutoa taarifa.
UGAIDI Watikisa Tena Morogoro......Watu Watano Wajeruhiwa Kwa Bomu, Vijana Wawili Wanaswa Na Kutoroka Kimafia

WATU watano akiwemo dereva wa gari linalotumiwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kilombero, David Ligazio ,Novatus Ngope (47), wamejeruhiwa vibaya na shambulio la kitu kinachodhaniwa ni bomu la kutupwa na mkono kutoka kwa watu wawili wasiofahamika walipokuwa kwenye sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani juzi.
 
Bomu hilo liliwajeruhi watu hao walipokuwa kwenye maadhimisho hayo yaliyofanyika katika kijiji cha Msolwa Ujamaa ,Kata ya Sanje ,wilayani Kilombero, mkoani Morogoro.
 
Dereva huyo anayeishi Ifakara anayeendesha gari la halmashauri lenye namba za usajili SM 10632 na wenzake baada ya kulipuliwa na bomu walikimbizwa Kituo cha Afya cha Nyandeo kilichopo Tarafa ya Kidatu ,baadaye walihamishiwa Hospitali Mtakatifu Kizito iliyopo Mikumi,wilayani Kilosa.
 
Mkuu wa wilaya ya Kilombero, Lephy Gembe alithibitisha jana kwa njia ya simu alipozungumza na mwandishi na kusema tukio hilo lilitokea majira ya saa 2:00 usiku wa Mei Mosi mwaka huu eneo la Kijiji cha Sanje.
 
Alisema vijana wawili wanaotuhumiwa kurusha mlipuko huo baada ya kuwajeruhi watu hao watano, walifanikiwa kukimbia kutoka eneo la tukio na Polisi inaendelea kuwasaka ili watiwe nguvuni.
 
Hata hivyo alisema, bado mpaka sasa taarifa kamili kuhusu chanzo na mazingira yake hakijafahamika na kwamba timu ya askari iliwasili eneo la tukio kwa ajili ya kukusanya taarifa na kuwasaka wahalifu hao.
 
Alisema inawezekana huo ni muendelezo wa matukio ya kihalifu kufuatia kukamatwa kwa watuhumiwa 12 waliokutwa na milipuko hatari na vitu mbalimbali zikiwemo sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ)Aprili 14, mwaka huu katika Kata hiyo ya Kidatu, wilayani Kilombero.
 
"Ni wiki chache zilizopita tumewakamata watu 12 na milipuko hatari na sare za jeshi , inawezekana kundi hili la kihalifu ni kubwa na wengine wameendelea kujificha msituni,” alisema Mkuu wa wilaya.
 
Tukio la mlipuko huo umetokea karibu na eneo ambapo hivi karibuni ,Polisi iliwakamata watu kumi wakiwa na milipuko 30,sare za jeshi ,majambia, risasi ,bendera zenye maandishi ya lugha ya kiarabu ,vitabu na madaftari wakiwa ndani ya msikiti wa Suni, Kidatu wilayani humo.
 
Kwa mujibu wa Mkuu wa wilaya hiyo, katika tukio hilo watu hao waliojeruhiwa ni pamoja dereva wa gari la halmashauri ya wilaya ambalo linatumiwa na Mwenyekiti wake.
 
“Pamoja na kumjeruhi dereva huyo pia gari limevunjwa kabisa kioo cha nyuma na kupasuliwa cha mbele kutokana na mlipuko huo,” alisisitiza Mkuu wa wilaya.
 
Hata hivyo alisema, timu ya maofisa wa vyombo vya ulinzi na usalama vya wilaya hiyo tayari vimelekea eneo la tukio hilo kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kina.
 
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Ligazio , akielezea tukio hilo alisema kuwa siku hiyo alikuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya siku ya wafanyakazi ngazi ya kata ya Sanje, akiwa ni diwani wa kata hiyo.
 
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo wa halmashauri, muda mfupi baadaye alikuja Mwenyekiti wa kitongoji hicho Joseph Mhenga akiambatana na vijana wawili .
 
Hata hivyo alisema, mwenyekiti huyo wa kitongoji kabla ya kufikishwa kwake alishawahoji walipotokea na walionekana si wenyeji wa eneo hilo kufuatia hofu walizokuwa wakizionesha.
 
Hata hivyo alisema vijana hao waliletwa kwake na mwenyekiti huyo wa kitongoji ili kutaka ushauri kuhusu vijana hao na alimwambia vijana hao wafikishwe katika kituo cha Polisi Kidatu kwa utaratibu mwingine wa kipolisi.
 
Kabla ya kupelekwa kituoni , vijana hao walifanyiwa upekuzi na askari wa mgambo, Thomas Manjole(54) ,mkazi wa Msolwa na walibainika kuwa na bomu.
 
Hata hivyo alisema , vijana hao walilitoa bomu hilo kiunoni na kulirusha kwenye gari la halmashauri ambalo linatumiwa na Mwenyekiti wa halmashauri hiyo.
 
Bomu hilo lilipolipuka likamjeruhi dereva wake aliyekuwa ndani ya gari pamoja na wengine wanne akiwemo askari mgambo.
 
 Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa halmashauri hiyo ambaye hakuwemo ndani ya gari aliwataja majeruhi hao ni dereva wake ,askari mgambo alikuwa akiwapekuwa vijana hao, Amos Msopole(29) na Azama Naniyunya(59) wote wakazi wa Kijiji cha Msolwa Ujumaa.
 
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji wa Kata ya Sanje , Hawa Ndachuwa ,alidai siku ya tukio watu wawili walikodi bodaboda kutoka Kata ya Kidatu na kuomba wapelekwe eneo la Kata ya Mkula .
 
Hata hivyo alidai kuwa, walipofika Msolwa Ujamaa, dereva wa bodaboda aliwashuku watu hao na kutaka aongezewe fedha za malipo kwani mapatano hayakulingana na umbali.
 
Alisema watu hao walikubali kumuongezea fedha na walimwomba kuwaonesha sehemu ya kutolea fedha na kuwapeleka eneo la kutolea fedha na kwamba mwendesha bodaboda huyo aliamua kuuarifu uongozi wa serikali ya kitongoji hicho.
 
Kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji wa Kata hiyo, baada ya wananchi kuwaona watu hao walipatwa na mshtuko kutokana na mavazi waliyovaa na kisha kuwaweka chini ya ulinzi na kuanza kuwapekua na ulifanyika chini ya ulinzi wa askari mgambo wa kijiji.
 
Hivyo alisema, wakati wanaendelea kupekuliwa, mtuhumiwa mmoja alikutwa na viberiti vya gesi na wakati upekuzi ukiendelea mtuhumiwa mwingine aligoma kutoa ushirikiano hali iliyowatia hofu zaidi wananchi ambapo walimwona akiwa na kitu amekihifadhi kiunoni.
 
Ofisa Mtendaji huyo alisema, wakati wanaendelea kupekuliwa mtuhumiwa wa kwanza alifanikiwa kukimbia na wakati wanajiandaa kumdhibiti wa pili alitoa kitu kama bomu na kurusha lilipo hilo gari la mwenyekiti na kutoa mlipuko mkubwa na yeye pia kutoroka.
 
Kutokana na mlipuko huo , askari mgambo Manjole ndiye alijeruhiwa vibaya kwa kuvunjika mguu na mkono huku dereva wa mwenyekiti Novatus akiumia begani na wote wanne kuchukuliwa na kupelekwa katika kituo cha afya cha Nyandeo .
 
Hata hivyo alisema , Polisi walifika eneo la tukio na kuwasiliana na wataalamu wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) waliopo eneo ya Kidatu ili kubaini bomu hilo huku wakiendelea kuwasaka watuhumiwa.
 
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mtakatifu Kizito, Maximilian Mwenda, alithibisha kupokea majeruhi wanne wa tukio hilo, kati yao mmoja akiwa na hali mbaya ambapo wengine wanaendelea kupatiwa matibabu na hali zao zinaendelea vyema.

Waziri wa Nishati na Madini Mh.George Simbachawene Awasimamisha Kazi Wahandisi Watatu TANESCO.


Waziri wa nishati na madini Mh.George Simbachawene ameagiza kusimamishwa kazi mara moja kwa wahandisi watatu wa shirika la umeme nchini TANESCO kutoka maeneo matatu jijini Dar es salaam baada ya wahandisi hao kushindwa kuwajibika ipasavyo ikiwa ni pamoja na  kutochukua hatua wanapopewa taarifa za kero za wananchi  kwenye maeneo wanayosimamia

 Wahandisi hao ni wa Temeke, Tazara na Tabata Magengeni, jijini Dar es Salaam, wanaodaiwa kusababishia Shirika hilo malalamiko kutoka kwa wananchi kila wakati.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Simbachewene alisema baadhi ya malalamiko yanayotolewa na wateja ni taarifa wanazotoa kuhusu nyaya za umeme na nguzo kuanguka bila kuchukuliwa hatua zozote.

Simbachewene alisema wajibu wa watendaji hao ni kushughulikia kero kama hizo sio wananchi waende kulalamika.

"Kila kukicha wanalalamikiwa Tanesco jana nilipiga simu Tazara na Tabata kuwajulisha kuna tatizo lakini hawajaenda, unakuta nyaya ya umeme imeanguka ina maana inasubiria fedha ya kigeni ndio itolewe hivi kazi yenu nini? Nguzo imeanguka mnajulishwa mwezi unapita hilo gari la emergency linafanya kazi gani," alihoji.

"Huyo mhandisi wa Tabata inawezekana hata hajui kitu, matatizo ni mengi na sidhani kama anafika na kuyafuatilia, hivyo naagiza chukueni hatua za kinidhamu ili iwe fundisho na kwa wengine," alisema.

Akizungumzia kero za kukatika umeme mara kwa mara alisema, umeme unakatika pasipo na sababu maalum. Waya umeanguka Temeke hadi watu wanakufa hakuna hatua zilizochukuliwa.

“Wananchi wamepiga simu hakuna hatua zilizochukuliwa mpaka watu wanakufa hatuwezi kuyanyamazia haya," alisema na kuongeza:
 
 “Sisi ni watumishi wa watanzania kwa leo naaza na hawa watatu wanatosha, wengine nitaendelea nao.”

Aidha, amepiga marufuku uegeshwaji wa magari ya Tanesco katika maeneo ya starehe kama baa, jambo ambalo alisema linalalamikiwa na wananchi.

Aliagiza vibarua wote walikokuwa wakitumiwa kwenye gari la dharura la Tanesco, kuajiriwa ili wasiwe wanachukua rushwa kwa wateja.

Alisema vibarua hao wamefanyakazi kwa muda mrefu bila kupewaajira na kila wakati ajira za Tanesco zinatangazwa.

Kuhusu tatizo la Luku, alisema hali imerudi kama kawaida na kuwataka kuendelea kununua huduma hiyo kupitia mitandao yote ya simu nchini.

Alisema chazo cha tatizo ni moja ya kampuni ya uwakala wa kuuza Luku kusimamishwa kutokana na kutokidhi viwango matakwa na taratibu za Mamlaka za Mapato (TRA),

Alifafanua kuwa kusimamishwa kwa kampuni hiyo kulilazimu mauzo yote yaliyokuwa yanapitia kampuni hiyo yapitie kwenye kampuni nyingine.

Alisema ili kukabiliana na hali hiyo, kampuni za simu zinazotoa huduma hiyo zililazimika kujiunga na mitandao mingine inayotoa huduma hiyo.

Alisema kwa sasa tatizo hilo limeshughulikiwa na huduma hiyo imeanza kutolewa kama kawaida.

Aidha, alisema mpango wa kujiunga  na kampuni nyingi zaidi zinazotoa huduma hiyo unafanyika ili kuondoa ukiritimba.

Akizungumzia azma ya kampuni ya Selcom ya kuishitaki Tanesco kwa kuvunja mkataba, alisema suala hilo haliwahusu kwani lipo upande wa TRA pamoja na Selcom.

KIKWETE ANAKUBALIKA

Mrema Ataka Rais Kikwete Aongeze Muda Wa Kuwa Rais ili Akamilishe Mchakato wa Katiba Inayopendekezwa



Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Augustino Mrema amesema hakuna ubaya Rais Jakaya Kikwete akiachwa kuongoza nchi kwa muda ili akamilishe mchakato wa Katiba Inayopendekezwa pamoja na Daftari la Kudumu la Wapigakura. 
 
Hivi karibuni viongozi wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), walidai kuwa Serikali na Tume ya Uchaguzi (NEC) inachelewesha uboreshaji wa Daftari la Wapigakura kwa lengo la kutaka kumwongezea Rais Kikwete muda wa kukaa Ikulu.
 
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema ni miezi mitatu imebaki kabla ya kampeni za uchaguzi, lakini mpaka sasa ratiba, majimbo yaliyogawanywa, watumishi wala vituo vya uchaguzi bado haviwekwa bayana na wala haifahamiki kazi ya uandikishaji katika Daftari la Wapigakura halijakamilika katika mikoa miwili.
 
“Hiyo ni hatari sana kwa Taifa. Tunaionya NEC isijaribu kufanya mbinu zitakazosababisha kuahirishwa kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu,” alisema Mbowe.
 
Akizungumza na mtandao  huu jana, Mrema alisema yeye ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza kutoa wazo la kutaka Rais Kikwete aongezewe muda zaidi wa kukaa Ikulu kwa kuwa kuna mambo mengi ambayo ni ya muhimu kwa Taifa yanayotakiwa kukamilika kabla ya Uchaguzi Mkuu.
 
Mrema alisema alitoa maoni hayo mwaka jana wakati viongozi wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) walipokutana na Rais Kikwete mjini Dodoma, lakini alishangaa kuona viongozi wengine wakipinga wazo hilo.
 
“Nilitoa ushauri Rais Kikwete akiwepo. Nilisema tusogeze Uchaguzi Mkuu mbele kwa miaka miwili ili atuachie nchi ikiwa salama, lakini wapinzani wamejiandaa kuingia Ikulu waliniona mimi kama bundi,” alisema Mrema.
 
Aliongeza kuwa hata Rais Kikwete hakuonekana kufurahishwa na hali hiyo iliyojitokeza baada ya kauli yake na kwamba, hivi sasa amebaini kuwa kiongozi huyo wa nchi hataki kuongezewa hata siku moja ya kuendelea kukaa Ikulu.
 
“Sema kwa sababu wenzangu wamejiandaa kuingia Ikulu mwaka huu, wameshawaandaa hata wake zao kuwa ‘ma-first lady’, lakini ukweli ni kwamba hata Katiba Inayopendekezwa ikipitishwa lazima kuwe na muda wa mpito.
 
“Simfanyii mtu kampeni, ninachosema ni kwamba, mambo hayajakamilika na tunataka yakamilike na michakato yote aliyeianzisha ni Rais Kikwete, ni vyema akaimaliza,” alisema Mrema.
 
Akihutubia kwenye sherehe ya maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani jijini Mwanza juzi, Rais Kikwete alisema hana mpango wa kuongeza muda kama baadhi ya wanasiasa wanavyodai.
 
“Nawashangaa wanaodai kuwa Serikali ina mpango wa kuongeza muda wa urais, sina mpango wa kufanya hivyo, tarehe imepangwa na uchaguzi utafanyika kwa mujibu wa Katiba,” alisema Rais Kikwete.

Jumamosi, 2 Mei 2015

Bodi ya Mikopo Ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Yaanza Kupokea Maombi ya Mikopo Kutoka Kwa Wanafunzi Kwa Mwaka Wa Masomo 2015/2016


Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) jana (Ijumaa, Mei 1, 2015) imetoa mwongozo kwa wanafunzi wahitaji wanaotarajia kuomba mikopo na ruzuku kwa ajili ya mwaka wa masomo 2015/2016 unaotarajiwa kuanza miezi michache ijayo.

Kwa mujibu wa mwongozo huo, ambao unapatikana katika tovuti ya Bodi (www.heslb.go.tz), waombaji wote wamepewa takribani miezi miwili kuwasilisha maombi yao kuanzia Jumatatu, Mei 4, 2015 hadi Jumanne, Juni 30, 2015.

Aidha, wanafunzi wote wahitaji wa mkopo na ruzuku wanapaswa kufanya na kuwasilisha maombi yao kwa njia ya mtandao kupitia mfumo maalum (Online Loans Application and Management System) ulioanzishwa na HESLB kwa ajili ya kupokea maombi hayo. Mfumo huo unapatikana kupitia tovuvi ya Bodi au kwa kufungua kiunganishi chake (http://olas.heslb.go.tz).

Pamoja na mambo mengine, mwongozo huo unafafanua kuwa waombaji wa mara ya kwanza (First Time Applicants) wanapaswa kulipa ada ya maombi ya Tshs 30,000/- kwa na kisha kutumia namba ya muamala (Transaction ID) kuingia katika mtandao na kuanza kujaza fomu za maombi.

“Waombaji wa mara ya kwanza wanapaswa kulipa ada ya maombi ya Tzs 30,000/- ambayo inalipwa mara moja tu na haitarudishwa kwa nia ya M-Pesa,” inasema sehemu ya mwongozo huo uloiotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo.

Aidha, mwongozo huo umesisitiza kuwa wanafunzi wenye mikopo na wanaoendelea na masomo katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu hawapaswi kuwasilisha maombi tena.

Bodi imewasihi waombaji na wadau wengine kuusoma na kuuzingatia muongozo huo wakati waote wanapofanya na kuwasilisha maombi.

HESLB ilianzishwa kwa sheria ya Bunge na 9 ya mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi mwezi Julai, 2005 ili, pamoja na majukumu mengine kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji waliodahiliwa katika taasisi za elimu ya juu. 
 
Aidha, jukumu jingine la Bodi ni kudai na kukusanya mikopo yote iliyotolewa kwa wahitimu wa taasisi za elimu ya juu kuanzia mwaka 1994 wakati Serikali ilipoanza kukopesha wanafunzi.
 
POSTED  BY; RASHID H.B

Ijumaa, 1 Mei 2015

AJIRA ZA WALIMU MAREKEBISHO

Breaking News: Marekebisho Yamekamilika.......Ajira za Walimu WAPYA 2015 Zimetoka Upya. Majina Yako hapa.

  A: Orodha ya Walimu na Mafundi Sanifu Maabara Ajira Mpya
 
Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI inatangaza ajira ya wahitimu wa mafunzo ya ualimu na mafundi sanifu maabara katika mamlaka ya Serikali za Mitaa kama ifuatavyo:-
 
i. walimu wa cheti (Daraja IIIA) kwa ajili ya shule za msingi 11,366;
 
ii. walimu wa stashahada 4,151 na shahada 12,490 kwa ajili ya shule za sekondari
 
iii. mafundi sanifu maabara 264 kwa ajili kusimamia maabara na kuandaa masomo ya sayansi kwa vitendo katika shule za sekondari


B: Utaratibu Ajira Mpya kwa Walimu na Mafundi Sanifu Maabara
Kila mwajiriwa mpya anatakiwa kuzingatia yafuatayo:-
 
i. walimu wenye sifa waliohitimu mafunzo kwa mwaka wa masomo 2013/14 wamepangwa pamoja na walimu wa sekondari wa masomo ya sayansi na hisabati waliohitimu miaka ya nyuma na wameomba kuajiriwa;
 
ii. kuripoti kuanzia tarehe 01 Mei hadi 09 Mei 2015 kwenye Ofisi za Wakurugenzi wa Halmashauri kwa ajili ya kuajiriwa na kupangwa vituo vya kazi;
 
iii. kuwasilisha vyeti halisi vya taaluma ya kuhitimu mafunzo, elimu ya sekondari, cheti cha kuzaliwa pamoja na nakala zake;
 
iv. hakutakuwa na mabadiliko ya vituo vya kazi; na
 
v. fedha za kujikimu kwa muda wa siku saba (7) na nauli ya usafiri wa magari (ground travel) zitatolewa kwenye halmashauri husika baada ya kuripoti.
 
Bonyeza  Hapo Chini Kuona  Orodha  Ya  Majina:

 
 
 
 
POSTED BY; RASHID HAMZA