Jumatano, 1 Aprili 2015

  KURA YA NDIYO ITAPITAKATIBA INAYOPENDEKEZWA

  • katiba-kura_95449.jpg

Marais Dkt. Jakaya Kikwete na Dkt Ali Shein mara baada ya kukabidhiwa Katiba inayopendekezwa Oktoba mwaka jana.
WAKATI siku za kupiga Kura ya Maoni zikikaribia, imebainika kuwa zaidi ya nusu ya Watanzania wataipigia kura ya Ndiyo Katiba Inayopendekezwa.
Aidha, imeelezwa mwito wa vyama vinavyounda umoja wa Ukawa wa kususa kura ya maoni haujawavutia wananchi wengi, hivyo wengi hawauungi mkono.
Hayo yamo katika taarifa ya matokeo ya utafiti uliofanywa na taasisi ya Twaweza kati ya Januari 27 na Februari 17 mwaka huu na kutolewa jana kupitia muhtasari wenye jina la “Kuelekea Kura ya Maoni ya Watanzania kuhusu Katiba Inayopendekezwa.”
Kwa mujibu wa taarifa ya utafiti huo uliosambazwa kwa vyombo vya habari na Mshauri wa Mawasiliano wa Twaweza, Risha Chande, muhtasari huu umetokana na takwimu za Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaofanyika kwa njia ya simu za mkononi.
Muhtasari huu unajumuisha maoni ya wananchi wa Tanzania Bara pekee juu ya Katiba Inayopendekezwa.
“Jumla ya wahojiwa 1,399 walipigiwa simu kati ya Januari 27 na Februari 17, 2015. Matokeo mengine yanatokana na duru la 5 la Sauti za Wananchi (iliyowahoji watu 1,708 kati ya Julai 16 na Julai 30, 2013) na duru la 14 la Sauti za Wananchi (iliyowahoji watu 1,550 kati ya Februari 12 na Machi 4, 2014).“Takwimu hizi zimetumika kufuatilia mwenendo wa muda mrefu. Ni muhimu kukumbuka kuwa mahojiano haya yalihusisha makundi yote ya wananchi wa Tanzania Bara.
Hata hivyo, maoni ya wananchi yanaonesha wazi mashaka yaliyopo katika mchakato mzima wa kuibadili Katiba, kwani mwezi mmoja tu kabla ya siku ya kupiga kura, uandikishaji wa wapiga kura haujakamilika.
Kutokana na hali hiyo, nusu ya wananchi (asilimia 47) wanafikiri uchaguzi mkuu ujao utafanyika chini ya Katiba mpya, lakini idadi ndogo (asilimia 30) inafikiri kuwa uchaguzi huo utafanyika chini ya Katiba ya sasa.
Kuhusu Ukawa kususa vikao vya Bunge la Katiba na ushawishi wake kwa wananchi kususa kura ya maoni, utafiti huo umeonesha: “Kati ya wananchi waliosikia minong’ono juu ya Ukawa kususa vikao vya Bunge la Katiba, asilimia 66 wanapinga hatua hiyo.
Asilimia 68 wanapinga ushawishi kwa wananchi kususa kura ya maoni na robo tatu (asilimia 75) ya wananchi wanasema hawatasusa kura ya maoni.” Aidan Eyakuze, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, alisema kuna “Kuna mambo matatu yanayojitokeza kutokana na maoni haya ya wananchi.
Jambo la kwanza ni kwamba kura ya ‘Ndiyo’ kwa Katiba Inayopendekezwa haina uhakika. Tofauti iliyopo ni finyu na wananchi wameonesha kwamba kura hii inaweza kubadilika wakati wote katika mchakato huu.
“Pili, kuna kilio kilicho wazi kuhusu umuhimu wa Katiba kusisitiza masuala ya uwazi na uwajibikaji. Wananchi wameunga mkono kwa nguvu zote vifungu vinavyoimarisha uwajibikaji. Changamoto kubwa zilizopo katika upatikanaji wa huduma za kijamii na kuwepo kwa tatizo kubwa la rushwa vyote vimekuwa na athari kubwa na wananchi wanatafuta njia za kuwawajibisha viongozi kwa matendo yao.
“Tatu, wananchi hawajashawishika kuchukua hatua za nguvu za kuleta mabadiliko. Mwito wa UKAWA wa kususa kura ya maoni haujawavutia na wananchi wengi hawauungi mkono. Mambo haya matatu yatakuwa changamoto kubwa kwa viongozi wa ngazi zote kuamini kwamba mawazo yao yanawakilisha maoni ya wananchi.”
Elvis Mushi, Mratibu wa Sauti za Wananchi alitoa maoni yake kuhusu matokeo hayo alisema: “Mashaka yaliyopo juu ya kukamilika kwa mchakato wa mabadiliko ya katiba na kubadilika kwa mwenendo wa mchakato huo kumesababisha mashaka kwa wananchi. Hali hii ndio inayosababisha maoni ya wananchi kugawanyika katikati kuhusu masuala yote muhimu.”
Askofu afunda viongozi wa dini
Viongozi wa dini wametakiwa kufundisha amani na upendo kwawaumini wao na si kuwahamasisha wananchi wasiipigie kura ya ndio Katiba ijayo, kwani hali hiyo imeelezwa itasababisha nchi kutokea mitafaruku ya wenyewe kwa wenyewe ikiwa hata viongozi wa dini nao watashiriki mambo ambayo hayawahusu.
Hayo alisema Askofu Mkuu wa Kanisa la Pentekoste Tanzania, Erasto Ikongo na ambaye ni Mwenyekiti wa Ushirika wa Wachungaji wa Kipentekoste Tanzania (PPT) alipokuwa anatoa tamko la kupinga kauli ya Jukwaa la Wakristo Tanzania (TCF), kuhusu kushikilia msimamo wao wa kushinikiza waumini kuipigia kura ya hapana Katiba Inayopendekezwa kwa kudai kuwa katiba hiyo imefika hapo ilipofika kwa njia ya ubabe na kukosa uadilifu.
Alisema viongozi wa dini wanatakiwa wabebe vitu vya Mungu na kuongelea masuala ya Mungu na si kuzungumzia yale ambayo hayawahusu.
“Viongozi wa dini waendelee kuhamasisha dini ili nchi yetu ibaki kuwa na amani na utulivu kama ilivyo sasa na si kuingilia masuala ya Katiba ambayo hayawahusu,” alisema na kuongeza kuwa, kama wao walikuwa na nia na Taifa hili wangebeba hoja moja tu ya inayohusu Mahakama ya Kadhi kwa vile ni suala la kidini na si kubeba hoja za Ukawa.
Pia, aliwataka viongozi wa dini wote waliokwenda bungeni Dodoma warudi kwani wanahamasisha waumini ambao ni wabunge vitu ambavyo vinaweza kupoteza amani nchini kwetu.
Awali, tamko la umoja huo lilitolewa juzi na kusainiwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Askofu Dk Alex Malasusa, Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa na Mwenyekiti wa Baraza la Maskofu wa KipentekosteTanzania (CPTC), Askofu Daniel Awet na kusema wao hawana hasira kama ambavyo watu wengine walivyotafsiri.CHANZO: HABARI LEO (Muro)

POSTED BY; RASHID HAMZA $ HASSAIN MTUNDA

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni