Jumatano, 1 Aprili 2015

WAZIRI MKUU AZUNGUMZI JUU KURA YA KATIBA

Waziri Mkuu Asema NEC Ndiyo Itakayoamua Iwapo Kura ya Maoni Ifanyike April 30 au La.......Awataka Wafanyabiashara Wasitshe Mgomo, Atoa Neo kuhusu Mahakama ya Kadhi

POSTED BY ANNASTAZIA RH

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ametoa ufafanuzi kuhusu suala la uandikishaji katika daftari la kudumu la wapigakura na siku maalum ya kupiga kura.

Amebainisha kuwa kutokana na hali ilivyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ndio itakayotoa ratiba kamili kuhusu hatma ya upigaji kura ya maoni.
 
Aidha, katika mgogoro na mgomo wa wafanyabiashara unaoendelea, amewataka wafungue maduka yao kwa kuwa tayari Serikali imeanza kushughulikia na kuyafanyia kazi malalamiko yao.
 
Akizungumza bungeni jana wakati wa kuhitimisha shughuli za mkutano wa 19 wa Bunge, alisema Serikali inatambua kuwa muda uliobaki kufikia siku ya kupiga kura ni mfupi, lakini Tume ndiyo yenye mamlaka kwa sasa ya kutoa ratiba kamili kuhusu tukio hilo.
 
“Tunatarajia Tume itatoa taarifa ya Ratiba itakayotumika kutuwezesha kukamilisha zoezi la uandikishaji pamoja na kutoa taarifa siku za hivi karibuni kuhusu upigaji wa Kura ya Maoni.  Ni dhahiri muda uliobaki kuanzia sasa ni mfupi lakini Tume ndiyo itakayotujulisha ratiba kamili,” alisisitiza.
 
Alisema Serikali kwa upande wake, imehakikisha fedha yote kwa ajili ya ununuzi wa BVR 8,000 zimelipwa kwa NEC  na matarajio ni kwamba kazi ya kuandikisha katika mikoa mingine itaanza na kuendelea kwa kasi.
 
Pia, alisema wakati  tume inajitahidi kufikia malengo hayo, Serikali inaendelea na mipango ya kuelimisha wananchi kupitia  redio, televisheni, magazeti mbalimbali kuhusu umuhimu wa Katiba inayopendekezwa ili kila mwananchi aielewe vizuri na kuweza kuipigia kura kwa matakwa yake mwenyewe bila kurubuniwa muda utakapofika.
 
Alisema tume hiyo imelenga kuandikisha wapiga kura milioni 21 na inakadiriwa kutakuwa na vituo 36,164, kila kituo kitaandikisha kwa siku saba hadi 11 kutokana na idadi ya watu na vituo vitafunguliwa kuanzia saa mbili hadi saa 12 jioni.
 
Akizungumzia suala la mgogoro wa wafanyabiashara Pinda, alisema katika kushughulikia suala hilo, Serikali ilikutana na wafanyabiashara hao na kukubaliana kuwa kwa sababu Serikali imeonesha nia ya kushughulikia malalamiko na changamoto zinazowakabili wafanyabiashara nchini ni  vizuri mgomo huo ukasitishwa.
 
“Serikali inathamini sana mchango wa wafanyabiashara katika kukuza Uchumi na kuchangia mapato ya Serikali. Napenda kuwahakikishia wafanyabiashara na wananchi wote kwamba, Serikali ipo tayari kukaa pamoja na wafanyabiashara kuzungumzia changamoto zinazowakabili na kuzipatia ufumbuzi wa haraka,” alisisitiza.
 
Akizungumzia suala la mauaji ya watu wenye ulemavu (albino), alisema itaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kiuchunguzi na kiupelelezi na kuwakamata wote wanaohusika na mauaji hayo yaliyojirudia tena nchini na kuwachukulia hatua za kisheria.
 
Alisema kwa sasa jumla ya watuhumiwa 181, wakiwemo Wanaume 171 na Wanawake 10 walikamatwa na kuhojiwa, kati yao watuhumiwa 133 walifikishwa mahakamani na kufunguliwa kesi za mauaji  na 46 kwa makosa ya kujeruhi.
 
 “Chanzo kikubwa cha mauaji hayo ni imani za kishirikina. Aidha, Matukio 41 kati ya 43 yametokea katika Ukanda wa Ziwa na Magharibi, kwani hadi sasa yametokea matukio 13 ya Mauaji Mwanza, Kagera matukio sita (6), Tabora matukio matano (5), Mara matukio manne (4), Geita matukio manne (4), Kigoma matukio Manne (4) Simiyu matukio matatu (3) na Shinyanga matukio mawili (2)” alisisitiza.
 
Kuhusu Mahakama ya Kadhi, alisema katika Mkutano wa 18 wa Bunge Serikali ilikusudia kuwasilisha bungeni Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali na sehemu ya tano ya muswada huo, ilikusudia kurekebisha Sheria ya Tamko la Sheria za Kiislamu.
 
Alisema muswada huo ni miongoni mwa Miswada minne ambayo haikupata nafasi ya kujadiliwa na Bunge. “Serikali itatumia fursa kuendelea kushirikisha wadau mbalimbali kwa lengo la kupanua uelewa juu ya maudhui na madhumuni ya Muswada huu”.
 
Pia, Waziri Mkuu alitoa pole kwa ajali zilizotokea na maafa yaliyotokana na mvua katika mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara na Kahama mkoani Shinyanga.
 
Spika wa Bunge, Anne Makinda, alilazimika kuvunja kikao cha asubuhi cha Bunge majira saa nne, baada ya wabunge wa vyama vya siasa vya upinzani kugoma mijadala mingine isiendelee hadi Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, atakapotoa kauli juu ya mustakabali wa uandikishwaji wapiga kura na hatima ya kura ya maoni.
 
Wabunge hao, pamoja na kujibiwa na Spika kuwa suala hilo, litatolewa maamuzi wakati Waziri Mkuu akihitimisha hoja ya kuahirisha Bunge, waligoma kukaa na wote wakasimama bungeni, na kuanza kuimba wakiwa wamewasha vipaza sauti huku wakigonga meza wakitaka hoja yao ijibiwe kwanza.
 
Chanzo cha vurugu kilianza pale, Mbunge wa Kisarawe Selemani Jafo (CCM), alipoomba mwongozo wa Spika, akitaka Bunge hilo lisitishe shughuli zilizopangwa na kujadili suala la kura ya maoni na namna ya kutengeneza Katiba ya mpito kwa ajili ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
 
Katika hoja yake hiyo, Jafo alisema kutokana na hali ilivyo ya uandikishaji katika daftari la kudumu la wapiga kura, ni wazi kura ya maoni haiwezi kufanyika Aprili 30, kama ilivypangwa.
Alisema ni wakati sasa Bunge hilo, lianze kujadili vipengele kama vile mgombea binafsi, kupinga matokeo ya urais mahakamani, kuwepo kwa tume huru ya uchaguzi na umri wa wabunge na Bunge ili viingizwe na kupitishwa kwenye kikao cha 20 cha Bunge ili Katiba ya Mpito ipitishwe.
 
Wakati Jafo akitoa maelezo yake kuhusu mwongozo huo, baadhi ya wabunge wa upinzani walikuwa wamesha vipaza sauti wakimpinga kwa madai kuwa, suala analotaka siyo la dharura.
 
Baada ya maelezo hayo ya Jafo, mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) naye aliomba mwongozo kwa kanuni ya 47 (1) inayohusu kusimamisha shughuli za Bunge zilizopangwa kwa siku hiyo ili jambo la dharura lijadiliwe.
 
“Mheshimiwa Spika uandikishaji wapiga kura nchi nzima, haujakamilika hata katika mkoa wa Njombe, Watanzania wapo katika sintofahamu ni lini wataandikishwa kwenye daftari la kudumu la wapiga kura,” alisema.
 
Alisema suala hilo ni la dharura na lilishaombewa miongozo zaidi ya mara moja bila majibu, hivyo si vyema Bunge hilo likaahirishwa bila kupatiwa majibu juu ya hatma ya uandikishaji huo wa wapiga kura na kura ya maoni.
 
“Tusitishe shughuli zote tuhakikishe tunajali, majibu yapatikane leo katika mkutano huu wa Bunge, nimeomba miongozo juu ya jambo hili mara mbili na mara zote Serikali haitoi majibu, sasa hakieleweki hapa hadi tupatiwe majibu,” alisema Mnyika.
 
Alisema “Waziri Mkuu yupo hapa anaweza kutoa majibu hapa na tukajadili jambo hili hapa,” alisema Mnyika.
 
Baada ya Mnyika kumaliza kuomba Mwongozo, Spika Makinda alibainisha kuwa hoja hiyo ya Mnyika haina tofauti na Jafo, na zote zipatiwa majibu na Waziri Mkuu wakati akitoa hoja ya kuahirisha Bunge.
 
Hata hivyo, jibu hilo la Spika halikukubaliwa na wabunge hao wa upinzani na ndipo mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali, alipowasha kipaza sauti bila ruhusa ya Spika na kusema “Hoja hii  haifanani na hoja ya kwanza, ile ya kwanza inataka majibu mkutano wa 20 na hoja hii ya pili inataka majibu mkutano huu.”
 
Wabunge wote wa upinzani wa vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi na CUF, walisimama na kuwasha vipaza sauti huku wakiongea kwa nguvu kuwa hoja hizo hazifanani na ni lazima hoja yao ipatiwe majibu kabla ya shughuli nyingine za Bunge kuendelea.
 
Machali alidakia tena na kusema, “Tunataka majibu, tumechoka kuburuzwa.”
 
Spika Makinda aliwajibu kwa kusema “Anawaburuza nani, nimewaambia kwamba swali lile litajibiwa leo (jana),au njooni basi nyie muendeshe hiki kikao, kama hamtaki kukubali majibu yangu tokeni nje.”
 
Huku wabunge hao wakiwa bado wamesimama na kuimba kuwa wanataka majibu, Spika alimwita Msemaji Kambi ya Upinzani kwenye Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, ili asome maoni ya kambi hiyo juu ya Mswada wa Sheria ya Miamala ya Kielektroniki ya mwaka 2014 na ule wa Makosa ya Kimtandao wa mwaka 2015, lakini hakutoka.
 
Aidha Spika aliendelea na kumtaka Katibu ataje shughuli inayofuata, ambaye aliisoma kwa mara ya kwanza Miswada ya Shera ya Kupata Habari wa mwaka 2015, wa Sheria Vyombo vya Habari wa mwaka 2015, wa Sheria ya Marekebisho ya Sheia ya Ushindani wa mwaka 2015 na wa Sheria ya Tume ya Walimu wa mwaka 2015.
 
Wakati akisema hivyo, baadhi ya wabunge wa upinzani waliendelea kusema kuwa alichofanya siyo utaratibu.
 
Baada ya hapo aliwafafanulia wabunge kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 47 kinasema, iwapo Spika ataridhika kwamba jambo hilo ni la dharura na lina maslahi kwa umma basi ataruhusu hoja litolewe kwa muda  dakika tano, na mjadala wa hoja utawezekana kama Spika ataridhika.
 
Pamoja na maelezo hayo, vurugu hizo za wabunge ziliendelea hadi alipoamua kuahirisha kikao hicho hadi jioni.
 
CHANZO MPEKUZI BLOG
 
 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni